Upinzani wataka makubaliano ya Ebola na Marekani kuwekwa wazi

Martin Mwanje
2 Min Read
Viongozi wa upinzani Eugene Wamalwa, Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka na Dkt. Fred Matiang'i

Upande wa upinzani sasa unaitaka serikali ya Kenya Kwanza kuweka wazi makubaliano yoyote yaliyofikiwa na Marekani kuhusiana na ugonjwa wa Ebola. 

Ukiongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, upande huo unasema ni haki ya kila Mkenya kufahamu yaliyomo kwenye makubaliano hayo.

“Tunatoa wito wa uchapishaji wa makubaliano yote, miongozo, ahadi na nyaraka husika juu ya mipango inayohusiana na ugonjwa wa Ebola, vituo, na matayarisho. Wakenya wana haki ya kujua kile kinachofanywa na serikali kwa jina lao,” alisema Musyoka kwenye taarifa leo Jumatano.

“Ulinzi wa afya ya umma ni wajibu wa kikatiba na suala la usalama wa taifa. Mipangilio yoyote inayohusisha moja ya magonjwa hatari zaidi duniani lazima ifanywe kwa kuzingatia viwango vya juu zaidi vya uwazi, uwajibikaji na ukaguzi wa umma.”

Upinzani ulitoa wito huo siku moja baada ya Rais  William Ruto kutetea ujenzi wa kituo cha kuwatenga wagonjwa wa Ebola raia wa Marekani katika kaunti ya Laikipia.

Akiwahutubia wanahabari juzi Jumatatu usiku huko Wajir, Ruto alisema kituo hicho kinalenga kuimarisha afya ya umma na uwezo wa nchi hii wa kukabiliana na changamoto ibuka.

Ruto alifananisha ujenzi wa kituo hicho na hatua zilizochukuliwa wakati wa janga la Covid-19, ambapo kituo cha kuwatenga walioambukizwa kilijengwa katika hospitali ya Nairobi kudhitibi ugonjwa huo.

Aliwasihi viongozi na wadau wengine kutoingiza siasa kwenye afya ya umma, huku akielezea kujitolea kwa serikali kulinda afya ya Wakenya wote.

Wakazi wa Nanyuki nao wamepinga vikali kuanzishwa kwa kituo cha karantini katika eneo hilo wakidai hatua hiyo itahatarisha maisha yao.

Share This Article