Maafisa wa polisi wamemkamata mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati katika kaunti ya Busia, kwenye operesheni iliyotekelezwa katikati ya jiji hilo.
Mshukiwa huyo, Ouma Dibogo Obobo mwenye umri wa miaka 37, alikamatwa baada ya polisi kupashwa habari kuhusu mienendo yake ya kutiliwa shaka.
Obobo alipatikana na bangi pamoja na mifuko iliyokuwa na bidhaa za unga zinazoaminika kuwa dawa za kulevya, ambazo zimepelekwa kwa maabara ili zitambuliwe.
Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imesema mshukiwa huyo ambaye ni mkazi wa kaunti ya Migori anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Busia huku uchunguzi ukiendelea.
“Idara ya DCI inasalia imara kwenye vita dhidi ya mihadarati, ikijitahidi kusambaratisha mitandao yote ya walanguzi wa mihadarati na kuwakamata wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu,” ilisema DCI.