Takriban watu 360 waliotekwa nyara na wanamgambo wa Boko Haram, wengi wao kutoka jamii ya Waislamu katika jimbo la Borno Kaskazini Mashariki mwa Nigeria mwezi Machi mwaka huu, wameachiliwa huru.
Hata hivyo, kungali na utata kuhusiana na jinsi mateka hao walivyoachiliwa. Jeshi la nchi hiyo lilisema lilitekeleza operesheni ya kijasusi kuwaokoa mateka hao na liliwapata wanamgambo hao kwa ghafla.
Hata hivyo, kundi moja katika eneo hilo la Borno South Youth Initiative, limedai kufanikisha kuachiliwa huru kwa mateka hao bila masharti, likiongeza kuwa idadi ya walioachiliwa ni watu 416.
Visa vya utekaji nyara vimeongezeka nchini Nigeria katika miaka ya hivi karibuni, licha ya kwamba ulipaji fidia ni haramu.
Kundi la Boko Haram, liliwateka nyara wasichana 200 wa shule kutoka kijiji cha Chibok mwaka 2014, huku 90 kati yao wakiwa hawajulikani waliko hadi sasa.