Kesi inayopinga kuondolewa afisini kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, itaamuliwa leo Jumatatu katika Mahakama Kuu ya Nairobi.
Majaji watatu Erick Ogola, Antony Mrima na Freda Mugambi, wanatarajiwa kutoa uamuzi huo siku chache baada ya pande zote kukamilisha mawasilisho yao tarehe 22 mwezi uliopita.
Hata hivyo, huku akisema ataheshimu uamuzi utakaotolewa na mahakama, kiongozi huyo wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), alidokeza kwamba atakata rufaa iwapo uamuzi huo utatolewa dhidi yake.
Akizungumza Jumapili katika kanisa la PCEA Muteero mtaani Karen, Gachagua alitoa wito kwa wafuasi wake kuwa watulivu bila kuzingatia matokeo ya uamuzi huo.
“Nawasihi wafuasi wangu kote nchini kuwa watulivu bila kuzingatia matokeo ya uamuzi wa mahakama. Rigathi ni mtu mpenda amani,” alisema Naibu huyo Rais wa zamani.
Gachagua alibanduliwa afisini Oktoba 17, 2024 baada ya Bunge la Seneti kuthibitisha mashtaka aliyolimbikiziwa na Bunge la Taifa.
Aliwasilisha kesi mahakamani akidai mchakato wa kumng’oa madarakani ulikiuka katiba na kwamba alinyimwa haki ya kusikilizwa.