Wagombea wa ubunge Ol Kalou wapiga kura, waelezea imani ya kushinda

Jumla ya wagombea 9 wanapigania kiti cha ubunge cha Ol Kalou kilichowachwa wazi kufuatia kifo cha mjumbe wa zamani wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho mwezi Machi mwaka huu.

Martin Mwanje
2 Min Read
Mgombea wa DCP Sammy Ngotho (aliyevalia fulana nyeupe) akiwahutubia wanahabari baada ya kupiga kura.

Wagombea mbalimbali wa kiti cha ubunge cha Ol Kalou tayari wamepiga kura huku wakielezea imani yao kwamba wataibuka washindi kwenye uchaguzi mdogo unaoandaliwa hii leo Alhamisi katika eneo bunge hilo. 

Mgombea wa UDA Samuel Muchina Nyagah alipiga kura katika shule ya msingi ya Huruma na kuelezea imani kwamba yuko tayari kutii uamuzi wa wakazi wa eneo hilo.

“Niko tayari kukubali matokeo. Watu wa Ol Kalou watazungumza kupitia kura, na chochote watakachoamua, tutakifuata,” alisema Nyagah muda mfupi baada ya kupiga kura.

Kwa upande mwingine, mgombea wa DCP Sammy Ngotho alipiga kura katika shule ya Ol Kalou Comprehensive na kuelezea imani kwamba ataibuka mshindi kwenye uchaguzi huo.

Wengine ambao wamepiga kura ni wagombea Mhandisi Wilson Kigwa wa chama cha Jubilee aliyepiga kura katika shule ya msingi ya Kandutura na Stephen Wanyoike Waithaka wa chama cha NLP aliyepiga kura katika shule ya msingi ya Gachwe.

Gavana wa Nyandarua Kiarie Badilisha naye alipiga kura katika shule ya msingi ya AC.

Uchaguzi huo mdogo umevutia jumla ya wagombea tisa ila ushindani unasemekana kuwa kati ya Nyagah wa UDA na Ngotho wa DCP.

Uchaguzi mdogo wa Ol Kalou unaandaliwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho mwezi Machi mwaka huu.

Share This Article