Weytan alaumu wanamgambo wa Jubaland kwa shambulio la Arabia

Watu sita waliuawa kwenye shambulizi hilo na wengine watatu wakajeruhiwa vibaya.

Marion Bosire
3 Min Read
Abdirahman Hussein Weytan, Mbunge wa Mandera Mashariki

Mbunge wa Mandera Mashariki, Abdirahman Hussein Weytan, ameshutumu wanamgambo wenye uhusiano na eneo la Jubaland nchini Somalia kwa shambulio la mauaji lililotokea kwenye barabara ya Mandera-Arabia.

Watu sita waliuawa kwenye shambulizi hilo na wengine watatu wakajeruhiwa vibaya.

Akizungumza katika kikao cha kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka 2026/2027 cha kamati ya bunge la taifa, Weytan alikosoa vyombo vya usalama kwa kile alichokitaja kuwa kushindwa kulinda wakazi licha ya uwepo mkubwa wa maafisa wa usalama katika eneo hilo.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja pamoja na maafisa wengine waandamizi wa usalama walikuwa wamefika mbele ya kamati hiyo kutetea mgao wao wa bajeti.

Mbunge huyo alipuuza madai kwamba shambulio hilo lilihusiana na migogoro ya kikoo, akisisitiza kuwa mauaji hayo yalikuwa kitendo cha kulipiza kisasi kilichotekelezwa na wanamgambo wenye silaha kufuatia operesheni ya hivi karibuni ya pamoja ya usalama katika eneo hilo.

Shambulio hilo lilitokea karibu na Kituo cha Omar Jillo wakati gari aina ya Nissan matatu lenye nambari ya usajili KAQ 914S lililokuwa likisafirisha wanafamilia kuelekea Mji wa Arabia lilivamiwa muda mfupi baada ya kupita eneo hilo.

Kulingana na mbunge huyo, maafisa wa usalama waliokuwa karibu hawakuchukua hatua yoyote licha ya uwepo wa kambi za Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) karibu na eneo hilo.

Weytan aliendelea kudai kwamba watu wenye silaha wanaohusishwa na vikosi vya Jubaland wanafanya shughuli zao waziwazi katika eneo hilo bila kuzuiwa na maafisa wa usalama wa Kenya.

“Jana, licha ya uwepo wa vikosi vyote vya usalama, mimi mwenyewe niliona wanajeshi wa Jubaland wakizunguka Omar Jillo wakiwa na silaha bila kuzuiwa,” alidai Weytan akiongeza kwamba hakuna anayewauliza chochote na wanapiga risasi watakavyo.

Hata hivyo, maafisa wa usalama waliwasilisha tathmini tofauti kuhusu tukio hilo, wakieleza kuwa ni hali ya kiusalama inayobadilika haraka na huenda ikahusishwa na uhalifu mpana pamoja na mivutano kati ya jamii.

Inspekta Jenerali Douglas Kanja alitangaza kuimarishwa kwa operesheni za usalama na uchunguzi kufuatia shambulio hilo la mauaji karibu na Arabia katika Kaunti ya Mandera.

Alisema Kamati ya Usalama ya Kaunti ya Mandera, pamoja na vyombo vyote husika vya usalama, imeagizwa kupitia mara moja tukio hilo, kutathmini hali ya usalama iliyopo na kuweka mikakati ya kuzuia hali hiyo kuendelea kuwa mbaya zaidi.

Mkuu huyo wa polisi alionya kuwa ingawa uchunguzi wa awali unaonyesha uwepo wa shughuli za kihalifu, hali hiyo inaweza kusababisha mzozo mkubwa zaidi ikiwa haitadhibitiwa kwa umakini.

Share This Article