Shambulio la Mandera: Oparesheni za usalama zaimarishwa

Mkuu wa Polisi Douglas Kanja alisema hayo katika kikao cha kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka wa 2026/2027 mbele ya kamati ya bunge

Marion Bosire
3 Min Read

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ametangaza kuimarishwa kwa operesheni za usalama na uchunguzi kufuatia shambulio la karibu na Arabia katika Kaunti ya Mandera. 

Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu sita na kuacha wengine kadhaa na majeraha.

Mkuu huyo wa Polisi alikuwa akizungumza katika kikao cha kujadili makadirio ya bajeti ya mwaka wa 2026/2027 mbele ya kamati ya bunge.

Alisema Kamati ya Usalama ya Kaunti ya Mandera na vyombo vyote husika vya usalama vilielekezwa mara moja kuangazia upya tukio hilo na kutathmini hali ya usalama iliyopo ili kuzuia hali kuendelea kuwa mbaya zaidi.

Shambulio hilo limeongeza taharuki katika eneo hilo huku kukiwa na wasiwasi kuhusu ukosefu wa usalama na uwezekano wa mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Kanja aliambia wabunge kuwa tathmini za awali zilionyesha kuwa tukio hilo ni la uhalifu, lakini akaonya kwamba hali hiyo iko katika hatari ya kugeuka kuwa mgogoro mkubwa wa kijamii kati ya jamii tofauti iwapo haitashughulikiwa kwa umakini.

“Ilibainika kuwa tukio hilo lilihusiana na uhalifu na kwamba hali ilikuwa ikiendelea kwa kasi kuelekea mgogoro mpana wa kijamii unaochochewa na uhalifu,” alisema Kanja.

Inspekta Jenerali huyo alifichua kuwa vyombo vya usalama tayari vimeanzisha uchunguzi wa kina ili kubaini sababu ya shambulio hilo, kuwatambua wahusika na kubaini iwapo kulikuwa na uratibu au ushawishi wa nje ulihusishwa na mauaji hayo.

Aidha alisema kuwa doria kali zimeimarishwa katika maeneo yaliyotambuliwa kuwa hatari kote Kaunti ya Mandera ili kuwapa wananchi walioathirika hakikisho la usalama, kuongeza uwepo wa maafisa wa usalama na kuzuia mashambulizi zaidi au vitendo vya kulipiza kisasi.

Kanja pia alifichua kuwa mamlaka zimeanzisha mashauriano na viongozi wa kisiasa, wazee wa koo, viongozi wa dini na wawakilishi wa jamii kutoka maeneo yaliyoathirika kama sehemu ya juhudi za kupunguza taharuki na kuhimiza mazungumzo pamoja na kuishi kwa amani.

“Mazungumzo na viongozi kutoka pande zote zilizoathirika yanaendelea kwa lengo la kuhimiza mazungumzo na kuzuia hali hiyo kuendelea kuwa mbaya zaidi,” alisema.

Mkuu huyo wa polisi aliongeza kuwa vyombo vya usalama vimeimarisha uratibu na mifumo ya kubadilishana taarifa kati ya vitengo mbalimbali pamoja na miundo ya kijamii ya maeneo husika ili kukabiliana na taarifa potofu na kuunga mkono juhudi za amani mashinani.

Kulingana na Kanja, ukusanyaji wa taarifa za kijasusi na oparesheni za ufuatiliaji pia zimeimarishwa katika maeneo yaliyo hatarini ili kugundua na kuzuia mashambulizi yoyote ya kulipiza kisasi au mipango ya makundi yenye silaha.

“Kwa sasa, mashirika yote husika ya serikali yameongeza operesheni za usalama na kuendeleza hatua zinazoongozwa na taarifa za kijasusi, zikijumuisha utekelezaji wa sheria pamoja na mbinu za mazungumzo ili kurejesha utulivu na kudumisha uthabiti ndani ya Kaunti ya Mandera,” alisema.

Share This Article