Tanzania imerejelea umuhimu wa ushirikiano wake wa muda mrefu wa kijeshi na China, ikisema ushirikiano huo umeimarisha uwezo wake wa kiusalama kupitia mafunzo, ubadilishanaji teknolojia na uwezeshaji.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 99 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China (PLA), yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Tanzania, Waziri wa Ulinzi Rhimo Nyansabo alisema ushirikiano huo ni nguzo kuu kwa uhusiano wa nchi hizo mbili, hususan katika kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto mpya za usalama zinazochipuza kote duniani.
Aidha, kulingana na waziri huyo, Tanzania na China zimejenga uhusiano imara wa ulinzi unaozingatia kuheshimiana, kuaminiana na dhamira ya pamoja ya kuendeleza amani.
Rhimo alisema ushirikiano huo utatekelezwa pia katika sekta ya elimu, afya, miundombinu, na maeneo mengine ya maendeleo.
Kwa upande wake, akizungumza kwenye hafla hiyo, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema uhusiano wa nchi hizo umejengwa kwenye msingi wa urafiki wa muda mrefu, kuaminiana na kusaidiana.
Wakati huo huo Mingjian, alithibitisha kuwa Jamhuri ya China itaendelea kusaidia juhudi za Tanzania za kuimarisha ulinzi na usalama.