Gloria Sekeiyan, ambaye ni mke wa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, ameaga dunia leo Jumamosi.
Kupitia ukurasa wa X, Seneta huyo alitangaza kufariki kwa Sekeiya, akisema kifo hicho kilisababishwa na mshuto wa moyo.
“Mke wangu Gloria Sekeiyan Khalwale, ameanguka ghafla na kufariki baada ya kukumbwa na mshuto wa moyo,” alisema Seneta huyo Jumamosi asubuhi.
Rais William Ruto na Mama Rachel Ruto, wametuma risala za rambirambi kuomboleza na fanilia ya Khalwale,
“Mama Rachel pamoja nami, tunatuma rambirambi zetu kwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale kufuatia kifo cha mke wake mpendwa Gloria Sekeiyan,” alisema Rais Ruto kwenye ukurasa wake wa X.
Kiongozi wa taifa alisema watasimama na familia ya Seneta huyo wakati huu mgumu wa majonzi, akidokeza kuwa kumpoteza mke, mshirika na mama kunaacha pengo kubwa.
“Tunamuomba Mungu kuipa familia hiyo nguvu, faraja na amani wanapomuomboleza mpendwa wao. Mungu aiweke roho yake mahali pema,” aliongeza Rais Ruto.