Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, amesema eneo la Magharibi mwa Kenya, limepiga hatua kubwa za kimaendeleo, chini ya serikali ya Rais William Ruto.
Alitaja ujenzi wa barabara unaoendelea na zile zilizokamilika, ujenzi wa viwanja vya michezo kama ule wa Kidudu kaunti ya Vihiga, uwanja wa Busia, Kakamega na Masinde Muliro kaunti ya Bungoma, uwekezaji kwenye hospitali ya Matibabu na Rufaa ya kaunti ya Vihiga, hospitali ya Kakamega level 6 na pendekezo la hospitali ya Bungoma level 6, kuwa baadhi ya miradi ambayo inawafaidi moja kwa moja wakazi wa eneo hilo la Magharibi.
Akizungumza aliposhiriki mkutano na Magavana kutoka eneo la Magharibi Jumamosi asubuhi, Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alisema uchukuzi wa watu na bidhaa pia umeimarishwa kupitia ujenzi wa viwanja vya ndege kama vile uwanja wa ndege wa Nasewa kaunti ya Busia, uwanja wa Webuye Matulo, ule wa Kakamega na uwanja wa ndege wa Kitale.
Kuhusu kubuni nafasi za ajira, Mudavadi alisema serikali imefanikisha uwekezaji katika kiwanda cha sukari cha Nzoia, ambacho kinatoa nafasi za ajira 3,000 na kuwafaidi wakulima 15,000.
Aidha, alisema wakazi pia wamefaidika pakubwa na viwanda vya pamba kama ile ya Luanda kaunti ya Busia, na ujenzi wa maeneo ya kiuchumi ya kaunti.
“Uwekezaji huu unapaswa kubuni nafasi zaidi kwa vijana wetu, masoko bora kwa wakulima, biashara dhabiti na huduma bora kwa wananchi,” alisema Mudavadi.
Magavana waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Fernandes Barasa (Kakamega), Ken Lusaka (Bungoma), Paul Otuoma ( Busia) na Wilber Otichilo (Vihiga).