Rais William Ruto ametangaza kwamba serikali itaanzisha ujenzi wa barabara ya safu mbili ya kutoka Athi River kupitia Kitengela hadi Isinya kabla ya mwisho wa mwaka 2026.
Akizungumza jana wakati wa ziara yake ya maendeleo katika kaunti ya Kajiado, kiongozi wa nchi alisema lengo la mradi huo ni kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo yenye shughuli nyingi.
Ruto alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele ya serikali ya ujenzi wa barabara chini ya Hazina ya Kitaifa wa Miundombinu, NIF.
Alitoa tangazo hilo alipokuwa akielezea miradi ya maendeleo inayoendelea na iliyopangwa kutekelezwa katika eneo la Kitengela.
Rais pia aliweka jiwe la msingi la miradi ya nyumba za bei nafuu ya Municipality na VET mjini Kitengela, ambayo inatarajiwa kujenga nyumba 2,850 kwa gharama ya shilingi bilioni 6.6.
Aidha, alikagua maendeleo ya ujenzi wa soko la kisasa la Kitengela, mradi wa gharama ya shilingi milioni 380 unaolenga kuwapatia wafanyabiashara mazingira bora na ya kisasa ya kufanya biashara.
Ruto alisema miradi hiyo ni sehemu ya ajenda pana ya serikali ya maendeleo, akisisitiza kuwa hatimaye Wakenya watapima viongozi kwa kuzingatia miradi na huduma wanazotekeleza.
Tangazo hilo linaongeza kasi katika mpango mpana wa serikali wa kupanua na kujenga barabara kuu zenye safu mbili kote nchini, kwa lengo la kuboresha ufanisi wa usafiri na kupunguza msongamano wa magari.