Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS imesifia mkutano wa kisiasa wa vuguvugu la Linda Mwananchi uliofanywa Jumapili wiki iliyopita katika uwanja wa Jacarada, Embakasi katika jiji la Nairobi.
Kwenye taarifa, msemaji wa NPS Muchira Nyaga ameuelezea mkutano huo kama uliofanywa kwa njia ya amani, heshima na kujizuia miongoni mwa waratibu, washiriki na maafisa wa usalama.
“Kile tulichoshuhudia Jumapili ni kile ambacho Huduma ya Taifa ya Polisi imekuwa ikihimiza wakati wote: kwamba tunaweza tukafurahia uhuru wetu wa kikatiba kwa amani na ndani ya sheria,” alisema Nyaga kwenye taarifa.
“Mkutano wa Jacarada ni shara tosha kwamba mikutano ya kisiasa inaweza ikafanyika bila vurugu na usumbufu wa utaratibu wa umma. Hivyo, tunawahimiza viongozi wote wa kisiasa, wafuasi na wadau kutumia mkutano huo kama mfano wa kuigwa wa mikutano ijayo.”
Vurugu na vitendo vya kihuni vimeshamiri katika mikutano mingi ya kisiasa katika siku za hivi karibuni nchini huku watu kadhaa wakijeruhiwa na hata wengine kufariki katika baddhi ya mikutano.