Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uganda National Unity Platform, NUP Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine, amekumbuka safari ya chama hicho kinapotimiza miaka 6.
Kupitia ujumbe aliochapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Wine alitaja safari hiyo kuwa ya kujitolea, uvumilivu na dhamira katika siasa za upinzani nchini Uganda.
Katika ujumbe wake, Kyagulanyi alisema chama cha NUP, kilichozinduliwa miaka sita iliyopita kama tawi la kisiasa la vuguvugu la People Power, kimepinga utabiri wa waliodai kuwa kingesambaratika ndani ya muda mfupi.
Alikumbuka wakosoaji walivyodharau chama hicho wakikiita “wimbi la kupita,” huku wakiwatuhumu wanachama wake kuwa wahuni na watu wasio na mwelekeo na kukiandalia kampeni endelevu za propaganda.
Licha ya changamoto hizo, Kyagulanyi alisema NUP kimekua na kuwa, kwa maelezo yake, nguvu madhubuti ya kupinga udikteta inayojitolea kutetea haki na hadhi ya kila raia wa Uganda.
Kiongozi huyo wa upinzani alisema maadhimisho hayo yanafanyika huku wanachama wa chama hico wakiwa na “mioyo mizito” wakikumbuka wanachama wanaoendelea kuzuiliwa, wanaodaiwa kuteswa na waliopoteza maisha katika harakati za kuleta mabadiliko ya kisiasa.
Alisisitiza kuwa ukandamizaji hautadhoofisha azma ya chama hicho akihimiza wafuasi kutokata tamaa, kwani vikwazo walivyokumbana navyo ni hatua za muda katika mapambano ya muda mrefu.
Alishukuru viongozi wa chama, matawi ya NUP ughaibuni na wafuasi wa ngazi za chini kwa kuendelea kuunga mkono chama hicho kwa miaka sita , akieleza imani kwamba “uhuru hauwezi kuzuilika.”