Moto wa Utumishi Academy: Maswali magumu yasubiri majibu

Martin Mwanje
2 Min Read

Nadhari ya wengi imeelekezwa kwa mamlaka za upelelezi wakati zikijibidiisha kupata ufumbuzi wa kilichosababisha mkasa wa moto kwenye shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru usiku wa kuamkia leo Alhamisi. 

Awali, kulikuwa na ripoti kwamba wanafunzi walishindwa kutoka bwenini baada ya kuzuka kwa moto kwa sababu milango ya bweni husika ilikataa kufunguka.

Swali ni je, ikiwa ni hivyo, nani aliyeufunga milango hiyo, na funguo zilikuwa wapi?

Na je, bweni hilo lilikuwa na mlezi au mtu mzima kama inavyotakiwa, kwa mujibu wa itikadi za usalama?

Kuna swali pia la madirisha yaliyowekwa kwenye bweni hilo. Kwenye picha zilizopigwa na wanahabari wetu, madirisha kwenye bweni hilo yanaonekana yakiwa yamewekwa chuma na vioo kwa namna ambayo mwanafunzi hawezi akatoroka patokeapo janga.

Wengi watasuburi kubaini ikiwa itikadi zingine za usalama ziliwekwa na utawala wa shule hiyo, ikiwa ni pamoja na kuweka vizima moto mabwenini.

Ilhali hii si mara ya kwanza kwa Kenya kukumbwa na mikasa ya moto ya aina hiyo.

Kuanzia kwa moto wa shule ya Bombolulu hadi wa hivi karibu kwenye Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha Academy, kumekuwa na mapendekezo mengi tu ya namna ya kuzifanya shule za malazi kuepukana na mkasa kama wa hivi karibuni huko Gilgil.

Akizungumza wakati akiwahutubia wanahabari katika shule ya Utumishi Girls Academy, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen alitoa wito wa utulivu na kuepukana na uvumi hadi uchunguzi kuhusiana na suala hilo utakapokamilika.

 

 

 

 

 

Share This Article