Rahab Mukami achaguliwa Rais wa chama cha wanawake bunge la Pan-Africa

Uongozi wa chama hicho ni wa mzunguko na sasa ni zamu ya Kenya kuongoza.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwakilishi wa kike wa Kaunti ya Nyeri, Rahab Mukami, amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Wanawake cha Bunge la Pan-Africa, hatua inayoiweka Kenya katika nafasi muhimu ya uongozi katika utawala wa bara.

Mukami ataongoza afisi ya chama hicho katika Bunge la Saba, kufuatia uchaguzi uliofanywa kwa kuzingatia kanuni ya mzunguko wa kikanda ya Umoja wa Afrika.

Ushindi wake unamweka katika nafasi ya juu ya jukwaa lenye ushawishi mkubwa, linalolenga kuendeleza uwakilishi na ushawishi wa wanawake barani Afrika.

Maafisa wapya waliochaguliwa wanaakisi utofauti wa bara, ambapo Aisha Adams wa Malawi aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza, Fatoumata Njai wa Gambia Makamu wa Rais wa Pili, Awatef Cheniti wa Tunisia Makamu wa Rais wa Tatu na Leocadie Ndacayizaba wa Burundi Makamu wa Rais wa Nne.

Chama cha Wanawake Wabunge Kenya kimesifia uchaguzi wa Mukami kikiutaja kuwa hatua ya kihistoria, kikieleza kuwa ni “wakati wa kujivunia kwa Kenya na uthibitisho wa uongozi wake wa kipekee.”

“Kupandishwa kwako kuongoza afisi ya chama cha Wanawake ya Bunge la Saba ni jambo la kujivunia kwa Kenya na uthibitisho wa uongozi wako bora na kujitolea kukuza sauti za wanawake katika utawala,” KEWOPA kilisema katika taarifa leo Jumanne.

Chama hicho kiliongeza kuwa jukumu jipya la Mukami linamweka katika nafasi ya kuendeleza usawa wa kijinsia na kuimarisha ushiriki wa wanawake katika maamuzi kote barani.

Kupanda kwa Mukami kunachangia kuimarika kwa hadhi yake ndani ya PAP. Mnamo 2024, Rais wa PAP Fortune Zephania Charumbira alimteua kuwa mshauri wake mkuu, hatua iliyoongeza zaidi ushawishi wake ndani ya chombo hicho cha bara.

Yeye ni miongoni mwa wawakilishi watano wa Kenya katika PAP, pamoja na Joseph Majimbo, Danson Mungatana, Esther Passaris na Margaret Kamar.

Ujumbe wa Kenya uliidhinishwa na Seneti mnamo Novemba 2022.

Share This Article