Aliyekuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameonya kwamba kutoaminiana ndiko changamoto kubwa zaidi inayodhoofisha juhudi za amani barani Afrika.
Akizungumza wakati wa Wiki ya Usuluhishaji ya Johannesburg mwaka 2026, Kenyatta alibainisha kwamba ingawa makubaliano yanaweza kufikiwa katika upatanishi wa migogoro, kuyadumisha ni jambo gumu zaidi kutokana na kuvunjika kwa imani kati ya serikali na raia na katika jamii.
Kenyatta alitoa kauli hizo katika kikao cha jopo la ngazi ya juu la Viongozi Wakuu Katika Mazungumzo: Uongozi na Utatuzi wa Migogoro Barani Afrika, lililowaleta pamoja marais wa zamani kushiriki maarifa kuhusu upatanishi na utawala.
Akitumia aliyoyaona nchini Sudan Kusini, Ethiopia na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uhuru alisisitiza kuwa utawala bora, ujumuishaji na usambazaji sawa wa rasilimali ni muhimu katika kutatua migogoro ya Afrika.
Alionya kuwa mgawanyiko ndani ya taasisi za bara umedhoofisha mshikamano ukilinganishwa na umoja wa awali wa upendo kwa Afrika, akisisitiza kwamba umoja si wazo tu, ni hitaji la lazima.
Kongamano hilo la siku tatu, lililoandaliwa na Taasisi ya Usuluhishaji ya Kusini mwa Afrika, liliwakutanisha wasuluhishaji, watunga sera, viongozi wa biashara na wasomi.
Kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Usuluhishaji katika mfumo wa dunia uliogawanyika: mustakabali wa biashara, uwekezaji na maendeleo endelevu.”
Washiriki wa ngazi ya juu walijumuisha marais wa zamani Joaquim Chissano, Goodluck Jonathan, na Ellen Johnson Sirleaf.