Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula wamewataka Wakenya kudumisha amani kufuatia visa kadhaa vya vurugu viliyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya kupinga bei za juu za mafuta.
Visa kadhaa vya uporaji pia viliripotiwa wakati wa maandamano hayo ya jana Jumatatu.
Prof. Kindiki anasema kuna haja ya Wakenya kudumisha amani wakati wote na viongozi kujiepusha na semi za uchochezi.
“Nawaomba hata kukiwa na matatizo au mazungumzo na serikali, tudumishe amani. Tusichochee wananchi au kuibia watu mali yao,” alisihi Naibu Rais.
Wito sawia umetolewa na Spika Wetang’ula.
“Mimi nawaomba, hii nchi tusiichezee. Amani ni ngumu kuifasiri lakini ni rahisi zaidi kutambua kukosekana kwake,” alishauri Wetang’ula.
Wahudumu wa sekta ya uchukuzi wa umma wametangaza kusitisha mgomo wao kwa siku moja ili kupisha mazungumzo na serikali.
Wakati huo, watu 55 waliokamatwa hiyo jana Jumatatu na juzi Jumapili mjini Machakos wakihusishwa na kushiriki na wengine kupanga maandamano mjini humo wamefikisha mahakamani hii leo.
34 kati yao walikamatwa hiyo jana na wamesomewa mashtaka ya kuweka mawe na vizuizi kwenye barabara kadhaa mjini Machakos na kutatiza uchukuzi.
Wameachiliwa kwa faini ya shilingi alfu 15 kila mmoja.
Kati ya 34 hao, mmoja alikubali mashtaka na kuhukumiwa kifungo cha mwezi mmoja au kulipa pesa taslimu elfu 15 za Kenya.
Mwingine mmoja alikosa kusomewa mashtaka kutokana na kuumia mguu na kutakiwa kurejea kortini tarehe 2 mwezi Julai mwaka huu kusomewa mashtaka baada ya kupata nafuu.
Aidha, wengine 22 wameachiliwa kwa dhamana ya shilingu elfu moja kila mmoja kwa kosa la kupanga maandamano usiku wa kuamkia siku ya Jumatatu.
Taarifa ya Martin Mwanje na Jonathan Mutiso