Jaji Gatembu Kairu amechaguliwa kuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa.
Anajaza pengo lililowacha wazi na Jaji Daniel Musinga ambaye kipindi chake cha kuhudumu cha miaka mitano kilimalizika.
Jaji Wanjiru Karanja amekuwa akikaimu wadhifa huo.
Jaji Kairu alipata kura 26 kati ya 41 kwenye uchaguzi uliowashirikisha majaji wa mahakama hiyo leo Jumatatu na kuchaguliwa kuiongoza.
“Pongezi Bw. Jaji Gatembu Kairu kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa. Ni chaguo ambalo ningefanya kama ningekuwa mpiga kura kwenye uchaguzi huo,” alisema wakili Nelson Havi kufuatia kuchaguliwa kwa Jaji Kairu.
Jaji Kairu naye alikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Majaji Patrick Omwenga Kiage, Agnes Kalekye Murgor na Lydia Awino Achode.
Nadhari sasa inaangazia mabadiliko atakayoleta kwenye mahakama hiyo muhimu katika kusikiliza rufaa zinazotoka Mahakama ya Juu na ambazo huwa ni moto wa kuotea mbali.
Rufaa za aina hiyo zinajumuisha ile ya Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua anayepinga kubanduliwa kwake madarakani.
Ingawa Mahakama Kuu kwenye uamuzi wake ilikiri kuwa hakupewa fursa ya kujitetea kabla ya kufurushwa kwake, iliendelea mbele na kumpa fidia ya shilingi milioni 50.
Ni fidia ambayo Gachagua ameipuuzilia mbali na kuapa kutafuta haki kwenye Mahakama ya Rufaa kwa misingi kwamba haki haiwezi ikafidiwa na kiasi chochote cha pesa.