Serikali yathibitisha vifo 18 kutokana na mafuriko

Maeneo kadhaa yaliyo katika hatari ya mafuriko huko Tana River yametambuliwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali imethibitisha vifo 18, vilivyosababishwa na mafuriko yanayotokana na mvua kubwa inayonyesha katika sehemu mbali mbali nchini.

Katika taarifa kuhusu hali hiyo, Wizara ya Usalama wa Taifa ilisema kwamba eneo lililoathirika pakubwa ni la mashariki mwa nchi ambapo watu 9 wamefariki kutokana na mafuriko.

Linafuatiwa na eneo la kati mwa nchi lililoripoti vifo vitatu, Pwani viwili, Nairobi viwili na idadi sawia katika eneo la Bonde la Ufa.

Taarifa hiyo vile vile ilitangaza utambuzi wa maeneo 59 katika Kaunti ya Tana River ambayo yako katika hatari kubwa ya mafuriko, hali inayodhihirisha kuongezeka kwa tishio katika mojawapo ya maeneo yaliyo hatarini zaidi nchini.

Maeneo mengi kati ya yale yaliyotambuliwa,hususan 32, yako katika Kaunti Ndogo ya Tana Delta, huku mengine yakisambaa katika kaunti ndogo za Tana River, Bangale, Tarasaa na Tana Kaskazini.

Onyo hili linafuatia wasiwasi unaoongezeka kuhusu kupanda kwa kina cha maji katika Bwawa la Seven Forks, ambalo maafisa wanasema linaweza kusababisha mafuriko makubwa katika maeneo ya chini ya Mto Tana.

Hata hivyo, hatari hii haiko Tana River pekee, kote nchini, maisha yamepotea kupitia kuzama, huku maji ya mafuriko yakipita kwa kasi katika maeneo ya makazi ya jamii mbalimbali.

Takriban watu 6,600 wameathiriwa, huku familia zikihamishwa na miundombinu muhimu kama barabara, shule na makazi kuharibika katika kaunti ndogo kadhaa.

Jamii zinazoishi kando ya Mto Tana na katika maeneo mengine yanayokumbwa na mafuriko huko Pwani, Kaskazini Mashariki, Nyanda za Juu, Bonde la Ufa na Nairobi zimeshauriwa kuwa macho na kuhamia maeneo ya juu mara tu watakaposhauriwa.

Serikali imesema makundi yanayojumuisha maafisa wa mashirika mbalimbali yanaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu na kuratibu juhudi za kutoa msaada.

Share This Article