Washukiwa wa wizi wa magari wakamatwa Nyeri

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa wa wizi wa magari wakamatwa kaunti ya Nyeri.

Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa watano wanaoaminika kuhusika na wizi wa magari na mifugo katika kaunti za Kirinyaga, Nyeri, na Murang’a.

Polisi walitekeleza operesheni ya kijasusi  baada ya habari kutolewa katika kituo cha polisi cha Kiaruhiu kuhusu kutoweka kwa gari aina ya Toyota Sienta, lenye nambari za usajili KCY 467A.

Kwenye operesheni hiyo, maafisa wa polisi walimkamata kiongozi wa genge hilo la majambazi Martin Ndegwa Kinyua, katika eneo la Kagicha alipokuwa akijiandaa kukutana na wenzake ili wauze gari hilo walilokuwa wameiba.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imesema baada ya mshukiwa huyo kuhojiwa, aliwapeleka polisi hadi katika eneo la Skuta Nyeri Mjini ambapo gari hilo lilipatikana likiwa na nambari bandia za usajili KDJ 765J.

Baadaye washirika wa Ndegwa walikamatwa wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Suceed lenye nambari za usajili KCS 523H, ambao ni Bernard Njeru Kimathi, Edwin Muchira Mwinga, Tobias Macharia Mwangi, na James Muthama Muriuki.

“Usiku huo ambao waliiba gari hilo, pia waliiba na kumchinja ng’ombe na kuuza nyama yake hatua inayozidisha biashara haramu ya nyama…. Imebainika kuwa genge hilo limehusika katika wizi wa mifugo kwenye kesi inayoendelea katika mahakama ya Kerugoya,” ilisema DCI.

Washukiwa wote wanazuiliwa korokoroni wakisubiri kufikishwa mahakamani.

TAGGED:
Share This Article