Bunge lalalamikia ongezeko la familia zinazoishi mitaani

Kamati ya bunge la taifa kuhusu hazina spesheli sasa inapendekeza matumizi ya njia za kupanga uzazi kati ya wanaoishi mitaani

Marion Bosire
2 Min Read
Fatuma Mohammed, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uhasibu wa Hazina Spesheli

Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu uhasibu wa hazina spesheli imelalamikia kile inachokitaja kuwa ongezeko la familia zinazoishi kwenye mitaa ya miji mbali mbali humu nchini.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa mwakilishi wa kaunti ya Migori bungeni Fatuma Zainab Mohammed ilikuwa imemwalika Afisa Mkuu Mtendaji wa hazina ya kurekebisha familia zinazoishi mitaani Caroline Towett kujibu maswali kadhaa ya kiusimamizi.

Wanachama wa kamati hiyo ya hazina spesheli walitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na hazina ya kurekebisha wanaoishi mitaani kuhakikisha kwamba familia hizo zinaondolewa huko kabisa.

Mbunge Charles Nguna wa Mwingi Magharibi, alisema kwamba familia za mitaani zinaongezeka kila kuchao na ipo haja ya kuwa na mipango ya kurekebisha wananchi hao.

Towett katika jibu lake alisema kwamba mara nyingi huwa wanashirikiana na vituo vya kurekebisha tabia ambapo watu wa familia za mitaani husajiliwa, kupokea mafunzo na kisha kurejeshwa kwenye familia zao.

“Lengo letu ni kuwaondoa mitaani, kuwabadilisha na kuwaunganisha tena na jamii zao,” alisema Towett katika jibu lake.

Wanachama wa kamati hiyo akiwemo mbunge wa Kipkelion Mashariki Joseph Cherorot, Catherine Omanyo wa kaunti ya Busia na hata Mwenyekiti Fatuma Mohamed walikubaliana kwamba ipo haja kwa familia hizo kupata mafunzo kuhusu njia za kupanga uzazi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa hazina ya kurekebisha familia zinazoishi mitaani alisema kwamba tayari kuna mpango ambapo kwa ushirikiano na washirika wake, wanatoa mafunzo ya upangaji uzazi kwa wanaoishi mitaani.

Hata hivyo Caroline Towett alikiri kwamba raslimali hazitoshi huku akipendekeza kwamba serikali za kaunti ziingilie kati na kupiga jeki shughuli hiyo.

Alikiri kwamba kwa wengine, kuishi mitaani ni kama biashara kwani wao hujipatia mapato kwa kuombaomba ambapo mtu mmoja anaweza kupokea hadi shilingi elfu 5 kwa siku kutoka kwa wahisani.

Msimamizi huyo wa hazina ya kurekebisha wanaoishi mitaani alilalamikia hatua ya baadhi ya wakenya kujitolea kulisha familia zinazoishi mitaani akisema kwamba hatua hii inahujumu juhudi zao za urekebishaji.

Hazina hiyo sasa inahimiza mkakati shirikishi wa wadau mbali mbali katika kushughulikia tatizo la familia zinazoishi mitaani.

Share This Article