Upatikanaji wa vitambulisho vya kitaifa unaongeza fursa, asema Katibu Omollo

Martin Mwanje
1 Min Read
Dkt. Raymond Omollo - Katibu wa Usalama wa Taifa

Mageuzi yanayoendelea yanayofanywa na serikali ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya kitaifa yanasaidia kuondoa vikwazo ambavyo vimewazuia Wakenya wengi kunufaika na huduma za serikali kwa miaka mingi iliyopita. 

Katibu wa Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo amesema kwa kupata vitambulisho hivyo, Wakenya hao sasa wanaweza wakapata fursa za maendeleo na kushiriki michakato ya kidemokrasia kinyume cha ilivyokuwa awali.

Akizungumza katika eneo la Ugunja, kaunti ya Siaya, Dkt. Omollo alisema Rais William Ruto ameagiza kuwa Wakenya wanaostahiki wawezeshwe kupata vitambulisho vya kitaifa bila vikwazo vyovyote.

“Upatikanaji wa vitambulisho vya kitaifa unahusu uraia, ujumuishaji na heshima. Hakuna Mkenya anapaswa kutengwa katika utoaji wa mipango ya serikali au ushiriki wa demokrasia kwa sababu anakosa kitambulisho cha kitaifa,” alisema Dkt. Omollo.

Alilalama kuwa idadi kubwa ya watu wazima katika maeneo mbalimbali kote nchini bado hawana vitambulisho vya kitaifa au kadi za kupigia kura, hali inayowazuia kupata fursa na huduma za serikali.

Dkt. Omollo lisema mpango unaoendelea unakusudia kuhakikisha kila Mkenya anahesabiwa, kuwakilishwa na kuweza kunufaika kutokana na mipango ya serikali.

 

Share This Article