Sehemu ya barabara ya Waiyaki kufungwa kwa muda wa miezi 3

Sehemu itakayoathiriwa ni eneo la Karuna Close na mzunguko wa magari wa Westlands, na itafungwa kwa muda kuanzia tarehe 25 mwezi Juni hadi tarehe  25 mwezi Septemba mwaka huu.

Tom Mathinji
1 Min Read
KeNHA kufunga sehemu ya barabara ya Waiyaki kwa muda wa miezi 3.

Halmashauri ya Taifa ya Usimamizi wa Barabara Kuu nchini (KeNHA) imetangaza kufungwa kwa muda kwa sehemu ya barabara ya Waiyaki Way jijini Nairobi.

Kulingana na KeNHA, sehemu ya barabara hiyo itafungwa kwa muda wa miezi mitatu ili kufanikisha  ujenzi na upanuzi  wa miundombinu ya usafiri katika eneo la Westlands.

Sehemu itakayoathiriwa ni eneo la Karuna Close na mzunguko wa magari wa Westlands, na itafungwa kwa muda kuanzia tarehe 25 mwezi Juni hadi tarehe  25 mwezi Septemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa ilani iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa KeNHA mhandisi Luka Kimeli, hatua hiyo itatoa fursa ya  upanuzi wa kivuko cha watembea kwa miguu katika eneo la Dunhill Towers pamoja na ujenzi wa kivuko kipya cha watembea kwa miguu katika mzunguko wa Westlands.

Wakati wa shughuli za ujenzi, usafiri utaelekezwa kupitia safu ya barabara jinsi ilivyobainishwa katika mpango wa usimamizi wa  shughuli za uchukuzi.

Aidha, kwenye ilani hiyo, madereva wameshauriwa wawe waangalifu na kufuata kanuni zote za trafiki katika maeneo yaliyoathirika.

Share This Article