Seneta wa kaunti ya Makueni, Daniel Maanzo ameomba taarifa kutoka kwa Kamati ya Seneti kuhusu Biashara, Uendelezaji wa Viwanda na Utalii kuhusu upatikanaji wa masoko ya maembe, choroko na mbaazi zinazozalishwa katika Kaunti ya Makueni.
Seneta Maanzo amesema kuwa Makueni ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa mazao hayo matatu, ambayo ni chanzo muhimu cha mapato na riziki kwa maelfu ya wakulima.
Maanzo alisema pia kwamba wakulima husika wana changamoto ya kuafikia viwango vinavyohitajika vya ubora na usalama wa mimea na mabadiliko makubwa ya bei wakati wa misimu ya mavuno mengi.
“Matokeo yake yamekuwa ni hasara kubwa baada ya mavuno na kupungua kwa mapato ya wakulima, hususan wale wanaolima maembe,” aliongeza.
Kamati hiyo inatarajiwa kuchunguza, hatua ambazo Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda inachukua ili kuhakikisha kunapatikana masoko ya uhakika ya ndani na ya kimataifa kwa maembe, choroko na mbaazi kutoka Kaunti ya Makueni.
Itatathmini pia juhudi zinazofanywa kuhakikisha wakulima wanapata bei za haki na zenye ushindani, pamoja na msaada unaotolewa kwa wakulima na vyama vya ushirika ili kukidhi viwango vya ubora, usalama wa chakula na usalama wa mimea vinavyohitajika katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Ombi jingine la Maanzo kwa Kamati hiyo ni kubaini hatua zilizowekwa kuhakikisha utulivu wa bei na kuwakinga wakulima dhidi ya hasara zinazotokana na mafuriko ya mazao sokoni wakati wa misimu ya mavuno mengi