Baraza la Magavana (CoG) limetishia kuwapiga kalamu wauguzi ambao mgomo wao umelemaza huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali za umma nchini.
Mgomo huo umeendelea kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita.
Mwenyekiti wa CoG ambaye pia ni Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi amelalamikia hatua ya wauguzi kukaidi amri ya mahakama ya kuwataka kurejea kazini.
“Tumekubaliana kwamba kila Gavana na Bodi yao ya Huduma ya Umma washughulikie suala la kutoheshimu amri ya mahakama kwa mujibu wa taratibu zilizopo za rasilimali watu,” alisema Gavana Abdullahi.
“Hivyo malalamiko yajayo ambayo tutashughulikia ni ya watu ambao wamefutwa kazi.”
Akizungumza wakati wa mkutano wa Baraza la Bajeti na Uchumi la Serikali Kuu na zile za Kaunti, IBEC, Gavana Abdullahi pia ametaja Mktaba wa Makubaliano (CBA) wa mwaka 2017 uliofikiwa kati ya Wauguzi na Magavana kuwa usiotekelezeka.

Amesema walishurutishwa kutia saini mkataba huo, ambao aliongeza kuwa gharama za utekelezaji wake haziwezi zikastahimilika.

Wauguzi wamekuwa kwenye mgomo kwa takriban mwezi mmoja wakishinikiza miongoni mwa mambo mengine, kutekelezwa kwa mkataba huo kama ilivyokubaliwa miaka tisa iliyopita.