Wakazi wa eneo la Magharibi wametakiwa kujiandikisha kama wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Rais William Ruto amelalamikia idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo ambao bado hawajajisajili kama wapiga kura licha ya kuwa na vitambulisho vya kitaifa.
“Maneno ya kupanga huko mbele, tutapangana. Sisi ndio mafundi ya hiyo maneno, msikuwe na wasiwasi. Lakini unajua sasa, kitu ya kwanza lazima mfanye, ili kupangana hapo mbele inahitaji kura,” alisema Rais Ruto alipotembelewa na klabu ya AFC Leopards katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatano.
“Lazima kila mtu ajiandikishe kwa kura. Kuna watu Western Kenya, watu milioni moja na nusu, wako na ID na hawana voters card, na wanasumbua sisi hapo kwa shopping centre. Mnatupigia makelele. Mnasumbua hapo kwa kupiga Isukuti, mtu unapiga Isukuti na hauna kura, unatusaidia na nini?”
Ruto akidokeza kuwa amezungumza na viongozi wa eneo la Magharibi wakiwemo Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na Magavana wa eneo hilo kuwahamasisha wakazi kujiandikisha kama wapiga kura.
Licha ya eneo hilo kuwa na idadi kubwa ya watu, ni wachache ambao hujitokeza kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu.