AFC Leopards yavuna vinono Ikulu

Miongoni mwa mambo mengine, Rais Ruto ameahidi kutoa shilingi milioni 25 zitakazotumiwa katika ufadhili wa klabu hiyo iliyomaliza ya pili msimu uliopita.

Martin Mwanje
2 Min Read
Wanaingwe wakiwa katika Ikulu ya Nairobi

Timu ya AFC Leopards ilicheka na vinono leo Jumanne ilipotembelea Ikulu ya Nairobi katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Mawaziri Salim Mvurya wa Michezo na Wycliffe Oparanya wa Vyama vya Ushirika. 

Mwenyeji wa timu hiyo, Rais William Ruto, akizungumza wakati wa ziara hiyo aliahidi kutoa shilingi  milioni 35 kwa Ingwe ili kusaidia kuipiga jeki klabu hiyo kifedha na kimiundombinu.

Rais Ruto pia aliahidi kutoa shilingi milioni 25 zitakazotumiwa katika ufadhili wa klabu hiyo, na kuongeza mapato ya ufadhili ya kila mwaka ya klabu hiyo kutoka shilingi milioni 75 hadi milioni 100.

Si hayo tu. Pia aliahidi msaada wa shilingi milioni 10 pesa taslimu, huku wachezaji wakigawiwa shilingi milioni 5 na zilizosalia kutumiwa kusajili wachezaji wapya kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa ligi kuu nchini.

“Mmeomba rasilimali za kuwasajili wachezaji wapya kabla ya kuanza kwa msimu ujao. Nitafanya kitu kuhusu hilo. Niwatapa shilingi milioni 10. Wachezaji watatia mfukoni shilingi milioni 5 na zilizosalia kutumiwa kusajili wachezaji wapya,” alisema Rais Ruto wakati akishangiliwa na Wanaingwe.

Kadhalika, Rais aliahidi kuwa serikali itaisaidia AFC Leopards kustawisha uwanja wa mafunzo ambao timu hiyo imekodi kwa kipindi cha miaka 15, na ambao maafisa wa klabu hiyo walisema kwa sasa hauko katika hali nzuri.

Na huku ikivuna vonono Ikulu, klabu ya AFC Leopards iliyomaliza ya pili nyuma ya Gor Mahia kwenye ligi kuu msimu uliopita na inayoonekana kutiwa motisha, imeahidi kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu ujao.

Share This Article