Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamewakamata washukiwa watatu wa ujambazi, wanaohusishwa na misururu ya wizi katika mtaa wa Westlands na maeneo mengine Jijini Nairobi.
Wa kwanza kukamatwa alikuwa Nimrod Khayeshe almaarufu Buda, aliyepatikana katika mtaa wa Kawangware, na baada ya kuhojiwa aliwapeleka maafisa hao kwenye maficho ya wenzake Vangelis Njungi, almaarufu Vangi na Patrick Kingato, ambao pia walitiwa nguvuni.
Kwenye operesheni hiyo ya kijasusi, maafisa hao walipata bastola aina ya Retay Falcon iliyokuwa na risasi tatu na pikipiki mbili zenye nambari za usajili KMGT 497W na KMHG 829H, zinazoaminika kutumika katika shughuli za ujambazi.
Watatu hao wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi, wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema operesheni hiyo inaashiria kujitolea kwa Idara hiyo kukabiliana na wahalifu na kusambaratisha mitandao yao kupitia operesheni za kijasusi kote nchini.