Rais William Ruto amezindua mpango wa Next Generation Youth Employment Programme (NextGen.KE), ambao ni mkakati wa serikali unaolenga kuwaunganisha vijana wa Kenya na ujuzi wa kikazi.
Mpango huo ni ushirikiano kati ya serkali ya Kenya, Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo (UNDP) na washirika wengine, ambao utawapiga jeki vijana 30,000 katika awamu ya kwanza, kupitia mpango wa uanagenzi wa sekta ya kibinafsi na ukuzaji wa ujuzi.
Akizungumza wakati wa uzindunzi wa mpango huo katika Ikulu ya Nairobi leo Ijumaa, Rais William Ruto alisema mpango wa uangenzi haupaswi kuchukuliwa kama ajira za muda mfupi, lakini kama njia ya vijana kupata ujuzi na mpito kutoka kwa hali ya masono hadi kuwa na mapato.
“Mpango wa uanagenzi sio ajira za muda mfupi. Ni daraja za mpito kati ya masomo na mapato, kati ya fursa na utekelezaji, na kati ya malengo na ufanisi,” alisema Rais Ruto.
Kupitia mpango wa NextGen, sekta ya kibinafsi itawachukuwa wanagenzi 15,000 watakaopata mapato, huku waliosalia wakipata mafunzo wa utaalam katika biashara, fedha na utayari wa sehemu za kazi.
Kulingana na kiongozi wa taifa, serikali itapanua mpango huo kuwafikia vijana 100,000, akidokeza kuwa shilingi bilioni mbili zimetengwa kwa mpango huo mwaka huu.
“Leo tunachukua hatua nyingine ya kijasiri. NextGen.KE ni ushirikiano mkubwa… katika muda wa miaka mitatu ijayo, mpango huu utachochea mageuzi ya kiuchumi ya vijana kwa kuwaunganisha na soko la ajira,” aliongeza Rais Ruto.