Zaidi ya wasafiri 80,000 wamechunguzwa dhidi ya ugonjwa wa Ebola katika viingilio tofauti vya Kenya, huku visa 56 vilivyotiliwa shaka vikipatikana bila ugonjwa huo.
Kwenye taarifa ya hivi punde, Wizara ya Afya imethibitisha kuwa wasafiri 3,969 wamechunguzwa ndani ya saa 24, huku mafisa wa 347 wakiwekwa katika hali ya tahadhari, taifa hili linapojitahidi kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na ugonjwa huo ambao umeshuhudiwa katika nchi jirani.
“Hadi leo watu zaidi ya 80,000 wamechunguzwa Ebola katika vituo tofauti vya kuingia hapa nchini……sampuli 56 zilizokusanywa kutoka kwa wasafiri waliotoka katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC, na Uganda hazikupatikana na ugonjwa huo,” ilisema taarifa hiyo ya Wizara ya Afya.
Kwenye taarifa hiyo, Waziri wa Afya Aden Duale alisema Kenya inasalia katika hatari ya kupata visa vya Ebola kutokana na uhusiano wake wa kibiashara, uchukuzi na watu walio kwenye mipaka na mataifa yaliyoathiriwa.
“Nawahakikishia Wakenya kwamba hadi kufikia Juni 5, 2026, Kenya haijanakili kisa chochote cha Ebola,” alisema Waziri huyo kwenye taarifa.
Aliongeza kuwa serikali imeimarisha uhamasishaji hasaa kwenye jamii za mpakani, wahudumu wa uchukuzi, wafanyakazi wa idara ya afya na makundi mengine yaliyo katika hatari ya kuambukizwa.
Kulingana na wizara hiyo zaidi ya wahudumu wa afya 1,759 wa kitaifa na wale wa kaunti wamepokea mafunzo kuhusu kukabiliana na ugonjwa huo.
Wakenya wamehimizwa kuzingatia viwango vya juu vya usafu na kutosambaza habari potovu kuhusu Ebola.