Maandalizi ya sherehe za mwaka huu za sikukuu ya Madaraka yanaendelea vyema kulingana na wizara ya mambo ya ndani na utawala wa kitaifa.
Katika taarifa iliyotiwa saini na katibu wa usalama wa taifa Raymond Omollo, wizara hiyo ilielezea kwamba hafla ya mwaka huu ya sikukuu hiyo ya Juni Mosi itaandaliwa katika kaunti ya Homa Bay.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Uchumi wa Buluu na Masuala ya Baharini” ishara ya kujitolea kwa serikali katika mikakati ya kutumia rasilimali za majini kwa maendeleo endelevu.
Uwanja wa Raila Odinga utakaotumika kwa maadhimisho hayo unakarabatiwa. Zaidi ya asilimia 70 ya kazi ya kurekebisha viti vya watakaohudhuria na jukwaa kuu imekamilika.
Ujenzi wa maeneo ya maegesho ya magari na upanuzi wa ukuta unaozunguka uwanja huo umefikia asilimia 60 na 80 mtawalia.
Maendeleo makubwa ya miundombinu yanaendelea katika Kaunti ya Homa Bay ili kuwezesha upatikanaji rahisi na ukuaji wa muda mrefu.
Zaidi ya kilomita 35 za barabara zinajengwa au kukarabatiwa.
Miradi muhimu ni pamoja na uboreshaji wa barabara ya Homa Bay Pier hadi uwanjani kwa usimamizi wa KeNHA, kazi ya kusawazisha barabara ya Wahambla–Imbo na Ruga–Lala chini ya KeRRA na uboreshaji wa barabara za kuingia eneo la maadhimisho kwa usimamizi wa KURA.
Wakati huo huo, makazi ya Kamishna wa Kaunti, ambayo yatatumika kwa ajili ya sherehe rasmi ya Kitaifa ya Bustani, yanafanyiwa ukarabati mkubwa. Maboresho ya nyumba kuu, huduma za nje na miundombinu yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 75.
Uwanja wa Ndege wa Kabunde pia unakarabatiwa ambapo upanuzi wa njia ya kurukia na kutua ndege umefikia asilimia 70 huku kazi ya uzio katika miisho ya njia hiyo ikiwa tayari imekamilika.
Jengo la abiria nalo linakarabatiwa pamoja na ujenzi wa sehemu mpya za kuegesha ndege na njia za taxi.
Katibu wa usalama wa taifa Raymond Omollo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Sherehe, amehakikishia wananchi kuwa serikali imejizatiti kuhakikisha sherehe hizi zinakuwa za mafanikio na zenye kukumbukwa.
Anatumai zitanyesha mshikamano na maendeleo ya taifa huku serikali ikitoa pongezi kwa ushirikiano kutoka kwa Serikali ya Kaunti ya Homa Bay na wenyeji.