Serikali yasifia G2G, yasema mfumo umesaidia kudhibiti bei za mafuta

Waziri Wandayi amesema mpangokazi huo unafanya kazi kama ilivyokusudiwa - ukihakikisha usambazaji thabiti na kupunguza hatari ya kupanda zaidi kwa bei za mafuta nchini.

Martin Mwanje
2 Min Read
Waziri wa Nishati, Opiyo Wandayi

Mfumo wa G2G umetekeleza jukumu muhimu katika kuhakikisha nchi hii inapata mafuta ya kutosha ya kukidhi mahitaji yake.  

Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi amesema licha ya changamoto zinazoshuhudiwa duniani kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati, mfumo huo umehakikisha usambazaji mafuta nchini Kenya unasalia thabiti kutoka kwa vyanzo mbalimbali.

“Mpangokazi wa G2G unafanya kazi kama ilivyokusudiwa – ukihakikisha usambazaji thabiti, ukipunguza hatari ya ubadilikaji wa bei za mafuta, na kutoa kinga dhidi ya kutokuwepo kwa uhakika duniani,” amesema Wandayi kwenye taarifa.

“Zaidi ya hilo, mpangokazi wa G2G pia umeiwezesha Kenya kupata mafuta kutoka kwa vyanzo mbalimbali. Shehena sasa zinapakiwa kutoka vyanzo mbalimbali vya kimataifa ikiwa ni pamoja na Ulaya, Pwani ya Ghuba ya Marekani, na eneo la Bahari Nyekundu.”

Waziri huyo amewahakikishia Wakenya kuwa nchi hii ina mafuta ya kutosha na kwamba serikali inafanya kila iwezalo kudhibiti bei ya bidhaa hiyo inayozidi kupanda duniani kote.

“Ingawa bei duniani kote zimepanda na kubadilika katika miezi ya hivi karibuni, mifumo ya Kenya imeundwa ili kukabiliana na athari za mabadiliko haya kwa njia ya kimuundo na inayoweza kutabiriwa.”

Serikali imetangaza kupunguzwa kwa mafuta ya dizeli kwa shilingi 10, na bei ya mafuta hayo itapunguzwa kwa shilingi 10 zaidi mwezi ujao kwa dhamira ya kuwakinga Wakenya dhidi ya athari za mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.

 

 

Share This Article