Kenya inaendelea kuimarisha juhudi zake za kukabiliana na Ebola, huku ikipokea vifaa vya kudhibiti ugonjwa huo hatari kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM.
Akipokea vifaa hivyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Ijumaa, Katibu katika Idara ya Afya ya Umma Mary Muthoni, alisema vifaa hivyo vitapiga jeki jitihada ya kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo katika vituo vya kuingia hapa nchini.
Vifaa hivyo ni pamoja na vifaa vya kupima joto mwilini, vieuzi, vitakasa mikono, glavu za kujikinga, sabuni ya maji, mapipa ya taka yenye rangi tofauti, dawa ya kusafisha, klorini na magwanda ya kuvalia.
“Tunaishukuru IOM kwa ushirikiano wake endelevu katika kuimarisha usalama wa Afya ya Umma,’ alisema Muthoni.
Aidha, Katibu huyo aliwahakikishia Wakenya kuwa taifa hili halijanakili kisa chochote cha Ebola, huku mifumo ya uchunguzi na kukabiliana na hatari za Afya ya Umma ikiwa imara.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa utawala wa Kenya na kaimu Mkuu wa Ujumbe wa IOM Faye Paath.