Ruto asaini amri ya kuwaondolea wakazi wa kaskazini mwa nchi hitaji la ukaguzi

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akitia saini amri ya kuondoa hitaji la ukaguzi wa wakazi wa kaskazini mwa nchi kabla ya kupewa nyaraka za utambulisho wa kitaifa

Wakazi wa eneo la kaskazini mwa nchi hawatahitaji kamwe kufanyiwa ukaguzi zaidi kabla ya kupewa nyaraka za utambulisho wa kitaifa.

Hii ni baada ya Rais William Ruto kutia saini amri ya kukomesha kitendo hicho ambacho amekitaja kuwa cha kibaguzi.

“Raia wenzetu kutoka kaskazini mwa Kenya hawatahitaji kamwe kupitia mateso yanayowakosea heshima ya kufanyiwa ukaguzi zaidi na kubaguliwa kikabila kabla ya kukabidhiwa nyaraka za utambulisho wa kitaifa,” alisema Ruto alipotia saini na kusoma amri hiyo katika uwanja wa Orahey mjini Wajir leo Jumatano.  

Katika kuondoa hitaji hilo, Rais alisema kila Mkenya yuko sawa mbele ya sheria na hafai kubaguliwa kwa misingi ya rangi, kabila au eneo analotoka.

Aliongeza kuwa uamuzi huo uliafikiwa kufuatia malalamiko mengi hasa kutoka kwa jamii ya Waisilamu yaliyowasilishwa kwa ofisi yake, bunge na taasisi zingine za serikali.

Awali, Rais Ruto aliyeandamana na Naibu wake Prof. Kithure Kindiki, Mawaziri na viongozi kutoka eneo hilo, alizindua mpango wa utoaji chanjo kwa mifugo.

Aliutaja mpango huo kuwa hatua muhimu itakayosababisha upatikanaji wa soko la kimataifa kwa manufaa ya nchi.

Aidha, alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali yake ukiwemo mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, 

Rais Ruto alianza ziara ya siku nne katika eneo la kaskazini mwa nchi jana Jumanne.

Website |  + posts
Share This Article