Rais Ruto: Serikali itafufua kiwanda cha Sukari cha Sony

Tom Mathinji
1 Min Read

Rais William Ruto ameahidi kufufua kiwanda cha sukari Sony kaunti ya  Migori ili kiweze kupata faida kama sehemu ya mpango mpana wa kuimarisha sekta ya sukari nchini.

Kiongozi huyo wa taifa alisema Serikali inalenga kutumia mikakati sawia na iliyotumiwa kufufua kiwanda cha sukari cha Mumias.

Kulingana na Rais Ruto, kundi la wasimamizi litateuliwa likiwa na maagizo ya kupea kipaumbele maslahi ya wakulima wa miwa katika operesheni za kampuni hiyo.

Rais aliyasema hayo wakati wa kuwekwa kwa jiwe la msingi kwa ujenzi wa taasisi ya mafunzo kuhusu mifugo katika eneo la Awendo kaunti ya Migori, litakalotumiwa kupiga jeki ufugaji nchini.

Rais pia alizindua mradi wa uunganishaji umeme wa Last Mile kaunti ya Migori, unaotarajiwa kuunganisha nyumba 25,000 kufikia Mwezi Disemba. Mradi huo utagharimu shilingi bilioni 1.9.

Alisema serikali inaimarisha uwezo wa kiuchumi wa ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na uvuvu, utalii na uchukuzi kubuni nafasi za ajira na kupunguza umaskini.

Aidha, Rais Ruto alikagua ujenzi wa soko la kisasa la Oria katika eneo bunge la Uriri.

Website |  + posts
Share This Article