Rais William Ruto ametia saini Mswada wa Fedha 2026 kuwa sheria siku chache baada ya mswada huo kupitishwa bungeni wiki jana.
Hafla ya kutia saini mswada huo ilifanyika leo Jumanne jioni katika Ikulu ya Nairobi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
Walijumuisha Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.
“Sheria hii haiongezi kodi zinazolipwa na Wakenya wa kawaida, badala yake, inaboresha usawa kwa kuimarisha utiifu, kuziba mianya, na kuhakikisha kila mtu na wafanyabiashara wanalipa ada wanazotakiwa kulipa kisheria,” alisema Rais Ruto wakati akizungumza baada ya kusaini mswada huo.
“Kwa kusaini Mswada wa Fedha 2026 kuwa Sheria ya Fedha ya 2026, na Sheria ya Ugavi wa Mapato 2026, Kenya sasa ina mpangokazi wa sheria na rasilimali za kufadhili vipaumbele vyake.”
Bunge la Taifa lilipitisha mswada huo Alhamisi wiki iliyopita ambapo wabunge 122 walipiga kura kuunga mkono mswada huo huku 40 wakiupinga.
Mswada huo ulipitishwa baada ya vipengee kadhaa kufanyiwa marekebisho yaliyopendekezwa na kamati ya Bunge la Taifa kuhusu fedha na mipango ya taifa.
Marekebisho hayo yalijumuisha kuondolewa au kufanyiwa marekebisho kwa mapendekezo kadhaa ya ushuru ambayo yalipingwa na wafanyabiashara, makundi ya kijamii na wananchi.
Serikali ilimeshikilia kuwa sheria hiyo inalenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato, huku ikiepuka ushuru utakaosababisha kuongezeka kwa gharama ya maisha.
Kupitishwa kwa mswada huo kulijiri baada ya wiki kadha za mijadala mikali bungeni, huku wabunge wakipigia darubini mikakati ya ushuru na mapato iliyopendekezwa na serikali.