Ni habari njema kwa maelfu ya wasafiri kufuatia taarifa kwamba upanuzi wa barabara kuu ya Nairobi-Nakuru utaanza mwezi ujao.
Hayo yamesemwa na Rais William Ruto wakati akiwahutubia wakazi wa kaunti ya Nakuru leo Jumatano.
“Hii barabara inatusumbua ya kwenda Nairobi, msongamano wa magari, watu wanalala kule Naivasha, wanalala Gilgil wakijaribu kutafuta barabara ya kwenda Nairobi ama wengine wanaenda Malaba, si ni kweli?” alisema Rais Ruto.
“Sasa tumekubaliana hii barabara yenu tunapanua. Tunaweka badala ya leni mbili, tunaweka leni sita, kutoka Nairobi mpaka hapa Nakuru. Na mimi nakuja kuanzisha huo mjengo mwezi ujao, mwezi wa kumi na moja.”
Rais Ruto akitumia fursa hiyo kuwaambia wakazi wa Nakuru kwamba njia pekee ya kubadilisha hadhi ya mji huo ni kupitia miradi ya maendeleo.
Barabara ya Nairobi-Nakuru hukumbwa na msongamano wa magari mara kwa mara hasa karibu na mji wa Naivasha na eneo la Gilgil.
Hali huwa mbaya zaidi hasa msimu wa sherehe za Krismasi kiasi kwamba baadhi ya wasafiri hulazimika kulala barabarani.
Wengi wanatumai kwamba upanuzi wa barabara hiyo utasaidia kurahisisha usafiri kwenye barabara hiyo na kuwaondolea wasafiri kero ambalo wamekumbana nalo kwa muda mrefu.
