Waziri Duale afika kortini, aonywa kwa kupuuza maagizo

Waziri Duale amejitetea akisema ujenzi wa kituo cha karantini mjini Nanyuki, kaunti ya Laikipia umesitishwa kusubiri uamuzi wa mahakama.

Martin Mwanje
2 Min Read
Aden Duale - Waziri wa Afya

Mahakama imetoa onyo kali kwa Waziri wa Afya Aden Duale ikimtaka kutopuuza maagizo yake. 

Duale alifika kizimbani leo Jumanne akikabiliwa na mashtaka ya kuidharau mahakama kutokana na ripoti za ujenzi wa kituo cha karantini mjini Nanyuki katika kaunti ya Laikipia.

Alikabiliwa na tishio la kufungwa jela kwa kuidharau mahakama.

Akijitetea, Waziri Duale aliiambia mahakama kuwa ujenzi wa kituo hicho umesitishwa kusubiri uamuzi wa kesi iliyowasilishwa mahakamani na kituo cha Katiba Institute na Chama cha Wanasheria nchini, LSK kupinga ujenzi huo.

Alielezea kuwa serikali ilinuia kujenga kituo hicho kwa sababu ya maslahi ya umma lakini ujenzi wake ulipigwa breki kufuatia maagizo ya mahakama.

Aidha, Waziri aliomba msamaha ikiwa kwa vyovyote vile alidharau maagizo ya mahakama akisema hakukusudia kufanya hivyo.

Ni kwa misingi hiyo Jaji wa Mahakama Kuu Patricia Nyaundi alifutilia mbali tishio la kumfunga jela Waziri huyo lakini kwa onyo kali kuwa upuuzaji wa maagizo ya mahakama siku zijazo utaadhibiwa vikali.

Jaji Nyaundi hasa alitaja hatua ya Duale kufika mahakamani haraka alipotakiwa kufanya hivyo akiitaja kuwa ishara anaheshimu mamlaka yake.

“Nimebaini kuwa Duale hakika ameheshimu mamlaka ya mahakama hii. Ameomba msamaha kama alivyotakiwa,” Jaji Nyaundi alisema katika uamuzi wake na kumwepushia Duale makali ya jela.

“Kwa sababu hii ni mara ya kwanza kwa Duale kuzungumzia hili, nitamwamini kwamba hakika haidharau mahakama. Kwa sababu hiyo, nitakubali msamaha wake, hasa ikizingatiwa ameelezea kinagaubaga kuwa anaheshimu mamlaka ya mahakama hii.”

Ujenzi wa kituo cha karantini hasa kwa lengo la kuwatibu raia wa Marekani waliobainika kuambukizwa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC uliibua shutuma kali kutoka kwa Wakenya.

Mjini Nanyuki, wakazi mara kadhaa walifanya maandamano kupinga ujenzi wa kituo hicho wakihofia kuwa kingefungua malango ya wao kuambukizwa.

Kenya haijaripoti hata kisa cha ugonjwa wa Ebola ambao umesababisha vifo vya watu zaidi ya 100 nchini DRC huku angalau mtu mmoja akiripotiwa kufariki nchini Uganda.

 

 

Share This Article