Maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wamemkamata mshukiwa aliyejisingizia kuwa afisa wa uchunguzi wa tume hiyo kwa madai ya kuitisha hongo kutoka kwa wananchi.
Mshukiwa huyo, Felix Manyaga Mogaka, alimfahamisha mkandarasi aliyepewa zabuni na serikali ya kaunti ya Narok kwamba kampuni yake ilikuwa ikichunguzwa kwa madai ya ufisadi. Baadaye walikutana katika hoteli moja ambapo mshukiwa aliitisha hongo ya shilingi milioni mbili ili kusimamisha uchunguzi huo.
Mkandarasi huyo alipiga ripoti kwa maafisa wa EACC ambao walianzisha uchunguzi mara moja, ambapo Mogaka alikamatwa akipokea shilingi 200,000 kama sehemu ya hongo hiyo.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa Mogaka sio mfanyakazi wa EACC.
Mshukiwa huyo kwa sasa anazuiliwa katika makao makuu ya EACC, akisubiri kufikishwa mahakamani.
Tume hiyo ilitoa wito kwa wananchi kuwaripoti watu wanaotumia jina la EACC kuwalaghai.