Wanajeshi wakamilisha mafunzo DRC

Kundi la kwanza la kikosi maalum cha Jeshi hilo limehitimisha rasmi mafunzo maalumu tayari kutumwa nyanjani.

Marion Bosire
1 Min Read

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FARDC limetangaza kwamba kundi la kwanza la kikosi maalum cha Jeshi hilo limehitimisha rasmi mafunzo.

Kulingana na FARDC mafunzo hayo yalikuwa ya kiwango cha juu na sasa kundi hilo liko tayari kupelekwa kwenye operesheni mbalimbali za ulinzi na usalama nchini DR Congo.

FARDC ilielezea kwamba wanajeshi hao walipitia mafunzo ya kina yaliyohusisha mbinu za kisasa za mapambano, operesheni za kijeshi, ulinzi wa maeneo muhimu pamoja na mbinu za kukabiliana na vitisho vinavyoikabili nchi hiyo.

Jeshi hilo limesema kuwa baada ya kukamilisha mafunzo hayo, kikosi hicho sasa kina uwezo kamili wa kutekeleza majukumu yake na kiko tayari kupelekwa katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kulinda mamlaka ya taifa, usalama wa wananchi na uadilifu wa mipaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kukamilika kwa mafunzo ya kikosi hicho kunatajwa kuwa sehemu ya juhudi zinazoendelea za serikali na uongozi wa kijeshi wa DRC za kuimarisha uwezo wa FARDC, kuongeza utayari wa vikosi vyake na kuboresha ufanisi wa operesheni dhidi ya changamoto za kiusalama zinazoendelea kuikabili nchi.

Share This Article