Bei ya mafuta yahusishwa na kupanda kwa bei ya saruji Tanzania

Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba, amesema kupanda kwa gharama za mafuta kumeongeza gharama za usafirishaji, na kuathiri moja kwa moja bei ya saruji na bidhaa nyingine.

Marion Bosire
2 Min Read
Mwigulu Nchemba, Waziri Mkuu wa Tanzania

Serikali ya Tanzania imesema kwamba ongezeko la bei ya mafuta ni mojawapo ya sababu kuu zinazoendelea kuchangia ongezeko la bei ya saruji katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kupanda kwa gharama za mafuta kumeongeza gharama za usafirishaji, hali ambayo imeathiri moja kwa moja bei ya saruji pamoja na bidhaa nyingine.

Nchemba aliyasema hayo akijibu swali la Mbunge wa neo la Kasulu Vijijini, Edibilly Kinyoma, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti bei ya saruji, baada ya kupanda kutoka Shilingi elfu 10, hadi elfu 25, katika baadhi ya maeneo.

“Kupanda kwa bei ya mafuta kumeongeza gharama za usafirishaji, hali ambayo imeathiri moja kwa moja bei ya saruji na bidhaa nyingine,” alisema Dkt. Nchemba.

Amesema Serikali imekuwa ikikutana na wadau wa sekta ya usafirishaji kwa lengo la kutafuta namna ya kupunguza gharama za usafirishaji ambazo zimekuwa zikichangia ongezeko la bei za bidhaa.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, tayari amekutana na wasafirishaji wa abiria na anatarajia kukutana pia na wasafirishaji wa mizigo ili kujadili changamoto zinazokabili sekta hiyo na namna ya kupunguza gharama za usafirishaji.

Hatua hiyo inalenga kusaidia kupunguza mzigo wa gharama unaowakabili wafanyabiashara na watumiaji bidhaa, huku Serikali hiyo ikiendelea kutafuta suluhisho la ongezeko la bei ya saruji na bidhaa nyingine.

Share This Article