Miradi ya TVET iliyokwamba Kisii yamulikwa na bunge

Miradi hiyo iko katika taasisi za TVET za Kitutu Chache Kusini na Mugirango Kusini.

Marion Bosire
2 Min Read
Dick Maungu, Mwenyekiti kamati ya bunge la taifa ya uwekezaji wa umma kuhusu utawala na elimu

Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Utawala na Elimu imeibua wasiwasi kuhusu miradi ya ujenzi ya thamani ya mamilioni ya fedha iliyokwama katika taasisi mbili za mafunzo ya kiufundi katika kaunti ya Kisii.

Kamati hiyo ilihoji kucheleweshwa, ongezeko la gharama kupitia marekebisho ya mikataba, ukosefu wa nyaraka na taarifa zinazokinzana kuhusu gharama na hali ya kukamilika kwa miradi katika taasisi hizo za Kitutu Chache Kusini na Mugirango Kusini.

Katika taasisi ya Kitutu Chache Kusini, mradi uliotolewa Aprili 2019 kwa gharama ya shilingi milioni 57.05 bado haujakamilika, licha ya shilingi milioni 50.97 kuwa tayari zimelipwa.

Gharama ya mradi huo baadaye iliongezwa hadi shilingi milioni 67.1, huku muda wa kukamilika ukiongezwa kwa wiki 139.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dick Maungu, alikosoa kuchelewa kwa mradi huo kwa miaka saba, akisema fedha za walipa kodi zimetumika katika kituo ambacho bado hakiwezi kutumiwa.

Wabunge pia walitaka maelezo kuhusu marekebisho ya mkataba, fedha za zuio na kushindwa kuwasilisha nyaraka za mkataba kwa wakaguzi.

Huko Mugirango Kusini, mradi wa shilingi milioni 55 ulikwama mwaka 2019 ukiwa umekamilika kwa asilimia 61.2 kutokana na kucheleweshwa kwa malipo.

Mkandarasi wa awali baadaye alisitisha mkataba kutokana na kukosa malipo na hivyo kusababisha kutolewa kwa mkataba mpya wa Sh21.58 milioni mwaka 2024.

Wabunge walihoji sababu ya kuhitajika kwa fedha zaidi na kuibua wasiwasi kuhusu marekebisho yasiyoidhinishwa na kazi za mwisho ambazo hazijakamilika.

Kamati iliagiza maafisa kurejea na faili kamili za miradi, makadirio ya gharama za ujenzi, idhini za marekebisho ya mikataba, rekodi za malipo na ratiba bayana za kukamilisha miradi.

Iliwaonya kuwa waliohusika na upotevu wowote wa fedha za umma watawajibishwa.

Share This Article