Serikali yaongeza jitihada za kuimarisha usalama mashinani

Katibu wa Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo amewataka maafisa wa utawala wa serikali kuu kufanikisha hilo kwa kuongeza ukusanyaji wa taarifa za kijasusi.

Martin Mwanje
2 Min Read
Dkt. Raymond Omollo - Katibu wa Usalama wa Kitaifa

Serikali kuu imeongeza maradufu jitihada za kuimarisha usalama katika maeneo ya mashinani nchini kote wakati pia ikiongeza mapambano dhidi ya matumizi ya mihadarati. 

Katibu wa Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo amewataka maafisa wa utawala wa serikali kuu kufanikisha hilo kwa kuongeza ukusanyaji wa taarifa za kijasusi, uhakikishaji wa usalama wa jamii na kuhakikisha raia waliotimiza umri wa kupata vitambulisho vya kitaifa wanapata stakabadhi hiyo muhimu.

Akizungumza alipokutana na maafisa wa utawala wa serikali kuu jijini Mombasa, Dkt. Omollo aliwaagiza makamishna wa kaunti na manaibu wao, machifu na manaibu wao na wazee wa vijiji kuimarisha ushirikiano na asasi za usalama na jamii za maeneo husika ili kutokomeza uhalifu wa kupangwa, magenge ya wahalifu, itikadi kali na tishio linaloongezeka la matumizi ya mihadarati.

“Mombasa ni moja ya vituo muhimu zaidi vya kiuchumi nchini. Chochote kinachofanyika hapa kinaathiri siyo tu eneo la Pwani bali pia nchi nzima,” alisema Dkt. Omollo.

“Hivyo, tunapaswa kulinda amani na usalama ili kubuni mazingira ambapo wafanyabiashara wananawiri, uwekezaji unakua, watalii wanatembelea nchi na watu wetu kupata fursa za kiuchumi.”

Dkt. Omollo alitaja matumizi ya mihadarati kuwa tishio linalowakabili vijana huku walanguzi wakiwa mwiba kwa familia na jamii kwa jumla.

Kwa misingi hiyo, alitoa wito wa ushirikiano kati ya jamii, Huduma ya Taifa ya Polisi, Idara ya Mahakama, shule, viongozi wa kidini na wazazi ili kuangamiza mitandao ya ulanguzi wa dawa za kulevya nchini.

 

Share This Article