Idara ya mahakama yajiandaa kwa uchaguzi

Maandalizi yanajumuisha utoaji mafunzo kwa Majaji na Maafisa wa Mahakama, uapisho na uteuzi wa Mahakimu Maalum na kuzipa kipaumbele kesi za uchaguzi.

Marion Bosire
2 Min Read
Jaji Daniel Musinga

Idara ya mahakama imeongeza juhudi katika maandalizi ya mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Maandalizi hayo yanajumuisha utoaji mafunzo kwa Majaji na Maafisa wa Mahakama,uapisho na uteuzi wa Mahakimu Maalum, pamoja na kuzipa kipaumbele kesi zinazohusiana na uchaguzi.

Akizungumza katika Mkutano wa Mashauriano wa Ngazi ya Juu kuhusu Usalama wa Uchaguzi, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Mahakama kuhusu Uchaguzi, JCE, Jaji Daniel Musinga, alisema idara hiyo imeanza kutekeleza mpango mpana wa maandalizi.

“Sehemu muhimu ya kazi hii ni kutoa mafunzo na kuendelea kujenga uwezo wa Majaji, Maafisa wa Mahakama na wafanyakazi wa Mahakama watakaohusika katika utoaji wa haki za uchaguzi,” alisema Jaji huyo.

Jaji Musinga alisema kuwa JCE inashirikiana na Ofisi ya Jaji Mkuu katika uteuzi na uchapishaji katika Gazeti Rasmi la Serikali wa Mahakimu Maalum, kama ilivyoainishwa chini ya kifungu cha 23 cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi.

Jaji Musinga alisisitiza tena kwamba “Mahakama imejizatiti kuzipa kipaumbele kesi zinazohusiana na uchaguzi, ikiwemo kesi za jinai,” akibainisha kuwa utatuzi wa kesi kwa wakati ni muhimu kwa haki ya msingi na utulivu wa kitaifa.

Mahakama pia itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa kesi na kuzingatia kikamilifu misingi ya Katiba na sheria kuhusu nidhamu na uwajibikaji katika kipindi cha uchaguzi.

Share This Article