Mawakili kuandamana leo kupinga mauaji ya wenzao

Vifo vya mawakili hao wawili vimeibua wasiwasi kuhusu usalama wa mawakili.

Marion Bosire
2 Min Read

Chama cha Wanasheria nchini Kenya, LSK leo Ijumaa kinaandaa maandamano ya kitaifa kulalamikia mauaji ya mawakili wawili wanachama wake.

Kimesema vifo hivyo ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya taaluma ya sheria na utawala wa sheria.

Maandamano hayo yanafanyika kufuatia kuthibitishwa kwa kifo cha wakili Esther Wairimu Keige baada ya kutafutwa kwa wiki kadhaa, siku mbili tu baada ya wakili Edward Muthee Kariuki kupatikana akiwa ameuawa nje ya makazi yake huko Athi River, Julai 5, 2026.

LSK imesema vifo hivyo vimeibua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa mawakili na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.

Chama hicho kinataka kuundwa kwa kundi la uchunguzi la mashirika mbalimbali kuchunguza mauaji hayo, kufanyika kwa ukaguzi wa kitaalamu wa masuala yenye utata kuhusu ardhi yaliyoshughulikiwa na Idara ya Sheria ya Huduma ya Misitu Kenya (KFS), kuimarishwa kwa usalama wa mawakili wanaohudumu katika taasisi za umma na kutolewa kwa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya uchunguzi.

Mawakili walioko Nairobi, watakusanyika katika maegesho ya Mahakama za Milimani saa tatu asubuhi kabla ya kuandamana kwa amani hadi makao makuu ya Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS kuwasilisha ombi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi.

Maandamano kama hayo pia yatafanyika katika matawi yote ya LSK nchini.

LSK imewahimiza mawakili, maafisa wa mahakama, wanafunzi wa sheria, mashirika ya kiraia na wananchi kuungana katika maandamano hayo kwa mshikamano, ikisema mashambulizi dhidi ya mawakili yanadhoofisha utoaji wa haki na utaratibu wa kikatiba.

Share This Article