Mwanamuziki wa Tanzania Rehema Chalamila, maarufu kama Ray C hataki kamwe kuitwa msanii mkongwe.
Huenda hili lilitokea wakati wa kuorodhesha waanzilishi wa muziki wa Bongo Flava, huku hafla ya kuadhimisha miaka 30 ya muziki huo wa Tanzania iliandaliwa usiku wa leo katika ukumbi wa Mlimani city.
“Biashara ya kuitana msanii wa zamani mnitue! Na Remmy Ongala mtasema wa lini? Na King Kiki je? Na Bi kidude? Wa mtondogoo au?? Semeni tu mlichelewa kuja mjini,” aliandika msanii huyo kwenye akaunti yake ya Instagram.
Msanii huyo ambaye kwa sasa anaishi nchini Ufaransa alisema ameshafanya uamuzi kwamba anarejelea muziki kabisa huku akihimiza mashabiki wake kumfuatilia kwenye YouTube anapotafuta kufikisha wafuasi laki moja huko.
Ray C wa umri wa miaka 44 sasa mzaliwa wa Iringa nchini Tanzania, alianza rasmi muziki mwaka 2001 na kufikia 2003 akazindua albamu yake ya kwanza kwa jina “Mapenzi Yangu”.
Ana albamu nyingine tatu ambazo ni ‘Na Wewe Milele; ya mwaka 2004, ‘Sogea Sogea’ ya mwaka 2006 na ‘Touch Me’ ya mwaka 2008.
Amekuwa akitoa nyimbo mpya mara kwa mara na sasa baada ya kimya cha miezi 9, ametoa kibao kipya kiitwacho, “Ongeza”.
Mwanadada huyo aliwahi kujipata kwenye tatizo la uraibu wa dawa ya kulevya aina ya heroin ambapo alipata usaidizi kutoka kwa Rais wa zamani Jakaya Kikwete wa kupata matibabu na hatimaye akashinda jinamizi hilo kabla ya kuhamia Ufaransa.