Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Kenya Nyota Ndogo amempongeza mwanamuziki mwenza Nadia Mukami, anapotimiza miaka 10 katika tasnia ya muziki.
Nyota ambaye kwa sasa yuko nchini Tanzania kwa tamasha ya miaka 30 ya muziki wa Bongo Flava, aliandika, “Hongera mpenzi wangu Nadia Mukami kwa kutimiza miaka 10 kwenye safari yako ya muziki”.
Aliendelea kueleza jinsi anavyofurahia kuwa mmoja wa watakaotumbuiza kwenye hafla ya kusherehekea miaka 10 ya Nadia Mukami katika eneo la burudani la Mass House, Agosti Mosi, 2026.
Nadia Mukami, anaadhimisha hatua muhimu baada ya kutimiza miaka 10 katika tasnia ya muziki, safari iliyogubikwa na uthabiti, maendeleo na mafanikio makubwa kupitia nyimbo zilizotamba katika chati mbalimbali.
Tangu alipoanza rasmi safari yake ya muziki, msanii huyo aliyeshinda tuzo mbalimbali amekua kutoka kuwa kipaji chipukizi hadi kuwa mmoja wa wanamuziki wanawake wanaotambulika zaidi Afrika Mashariki.
Akijulikana kwa nyimbo maarufu zinazochanganya mtindo wa Afro-pop na ladha ya kisasa ya muziki wa Kiafrika, Nadia amejijengea mashabiki waaminifu kupitia kazi zake zinazowavutia watu wa rika mbalimbali.
Safari yake ya muziki pia imejengwa kupitia ushirikiano na wasanii mashuhuri wa Afrika Mashariki, jambo lililopanua ushawishi wake nje ya mipaka ya Kenya.
Kando na Nyota ndogo kutakuwa na wasanii wengine kwenye sherehe hiyo kama Sanaipei Tande, Maandy, Ssaru, Bahati, Dufla Diligon, Fena Gitu na wengine wengi.