Serikali haitaruhusu maadhimisho ya maandamano ya vijana wa Gen Z Juni 25 kutumiwa kuzua vurugu nchini wala kuharibu mali ya umma.
Rais William Ruto amesema siku hiyo, kinyume cha wanaotaka kila kitu kusitishwa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa maandamano ya vijana wa Gen Z mwaka jana, shughuli zitaendelea kama kawaida.
“Kitu kimoja ambacho hakitafanyika, ni kwamba watu watakusanyika kuharibu mali, au kuzua vurugu au machafuko, hilo halitafanyika” alionya Rais Ruto.
“Watoto wataenda shuleni kwa sababu hiyo ni haki yao kwenda shuleni, wafanyakazi wataenda kazini kwa sababu hivyo ndivyo tunavyoongeza uzalishaji wa nchi yetu, na wafanyabishara wataenda na kufungua biashara zao na kukuza uchumi wetu. Na wakulima pia, na kila mtu ili kulifanya taifa letu kusonga mbele.”
Rais Ruto aliyasema hayo alipohutubia kongamano la kitaifa la uzalishaji na utendaji kazi katika chuo cha mafunzo ya serikali jijini Nairobi leo Ijumaa.
Jana Alhamisi, Gavana wa Siaya James Orengo aliwaongoza viongozi wengine kuelekea hadi jumba la Jogoo wakiitaka Idara ya Polisi kuwaruhusu kufanya maadhimisho ya maandamano ya Gen Z Juni 25.
Polisi waliidhinisha ombi lao ila kwa masharti kwamba maandamano hayo yatakuwa ya amani yasiyokuwa hata na chembe ya vurugu wala visa vya uporaji.
Waandalizi wa maandamano hayo wamenukuliwa wakiwataka Wakenya kusalia nyumbani siku hiyo.