Rais William Ruto amesema upatikanaji wa haki kwa haraka umetajwa kuwa hatua inayochochea ukuaji wa uchumi na ufanisi wa taifa.
Kiongozi wa taifa ameyasema hayo leo Ijumaa alipokuwa akihutubia kongamano la tatu la Majaji Wakuu wa Afrika kuhusu njia mbadala za upatikanaji haki.
Kwenye mkutano huo, Rais Ruto alipigia debe mfumo mbadala wa kutatua mizozo akisema umetumika kwa muda mrefu barani Afrika.
“Barani Afrika, mfumo mbadala wa upatikanaji wa haki, sio tu mfumo mbadala. Mazungumzo yamekuwa nguzo ya upatikanaji wa haki,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto alidokeza kuwa kile ambacho ulimwengu umegundua, bara Afrika limekuwa liutekeleza kutoka vizazi hadi vizazi.
Aidha, alisema mfumo mbadala wa upatikanaji wa haki uliwekwa kwenye katiba ya Kenya ya mwaka 2010 ili kufanikisha kupatikana kwa haki kupitia maridhiano, mapatano, na usuluhishaji wa mizozo kupitia njia za kitamaduni.
“Tunapaswa kusuluhisha kesi zetu barani Afrika na kwa kupitia taasisi za barani humu na majaji ambao wanafahamu maswala yetu,” aliongeza kiongozi wa taifa.
Wakati huo huo Ruto alisema Idara ya Mahakama imeongezewa bajeti ili iweze kutimiza malengo yake.