Wachekeshaji wapokea mafunzo Rwanda

yalilenga kuboresha ujuzi wao na kuhamasisha uwasilishaji wa vichekesho kwa njia ya kitaalamu zaidi.

Marion Bosire
2 Min Read

Wachekeshaji wa umri mdogo nchini Rwanda wamepokea mafunzo maalum kwa hisani ya waandalizi wa onyesho la vichekesho la ‘Gen-Z Comedy Show’.

Mafunzo hayo ya siku tatu, yalilenga kuboresha ujuzi wa wachekeshaji na kuhamasisha uwasilishaji wa vichekesho kwa njia ya kitaalamu zaidi.

Mpango huo uliofanyika kati ya Agosti 31 na Septemba 2, uliangazia uandishi wa vichekesho, mbinu za uigizaji na namna ya kushirikisha hadhira bila kuwafanyia mzaha watu binafsi wanaohudhuria onyesho.

Mwanzilishi wa onyesho hilo, Merci Ndaruhutse, alisema mpango huo unalenga kujenga mazingira yenye heshima zaidi kwa wachekeshaji na hadhira.

Alikiri kuwa baadhi ya wachekeshaji wamewahi kutoa kauli zisizofaa kuhusu watazamaji, lakini akasisitiza kuwa mafunzo hayo hayakuandaliwa kutokana na tukio la hivi karibuni lililomhusisha mfanyabiashara Kate Bashabe.

Bashabe alihudhuria onyesho hilo Agosti 27, lakini inaripotiwa aliondoka muda mfupi baada ya mchekeshaji Dudu kutoa kauli zilizomkera.

Merci alisema Bashabe aliondoka kutokana na mipango mingine, huku akikiri umuhimu wa kuzuia vichekesho visivyofaa.

Wachekeshaji wenye uzoefu, akiwemo Arthur Nkusi, Hervé Kimenyi, Michael Sengazi na Atome, walihusika katika kutoa mafunzo hayo, huku waandaaji wakipanga kikao kingine wiki ijayo.

Gen-Z Comedy Show, ilianzishwa mwaka 2022 na imekua kutoka jukwaa la wachekeshaji chipukizi na kuwa tukio maarufu la burudani jijini Kigali, likivutia wachekeshaji, watu mashuhuri na viongozi wa umma.

Share This Article